Kumbukumbu hizo ambazo ziko wazi kwa umma katika tovuti ya White House zinaonyesha kuwa, Dakta Kevin Cannard alitembelea White House mara nane kuanzia Agosti mwaka jana hadi Machi mwaka huu.
Wasifu wa Cannard kwenye LinkedIn unaonyesha kuwa ni daktari wa neva anayesaidia Kitengo cha Matibabu cha White House. Wakati huo huo waraka mwingine wa umma kwenye wavuti ya wataalamu wa matibabu ya Doximity unasema Dakta Cannard amekuwa akitibu wagonjwa wa Parkinson wa hatua ya awali.
Ziara hizo nane za dakta Kevin Cannard huko White House zinajumuisha kukutana kwake na daktari mwingine wa Joe Biden, Dakta Kevin O'Connor mwezi Januari mwaka huu katika kliniki ya White House. Dakta Cannard pia alikwenda White House mwezi Machi mwaka huu ambako alifanya mazungumzo na Megan Nasworthy afisa wa masuala ya uhusiano wa White House. Ziara za dakta huyo wa neva zilifuatiwa na nyingine kadhaa.
Karine Jean- Pierre, msemaji wa White House amekanusha kuwa Biden anapatiwa matibabu ya ugonjwa wa Parkinson huku akikataa kujibu maswali aliyoulizwa kuhusu ziara hizo za Dakta Kevin Cannard.
Alkhamisi iliyopita, Biden katika mdahalo wa urais na Donald Trump alionekana kusitasita na kuzubaa mara kwa mara, na pia kuparaganyika kimawazo, jambo lililoibua wasiwasi zaidi kuhusu ukongwe na umri wake mkubwa.Hii ni katika hali ambayo, uchunguzi wa maoni uliofanywa na mtandao wa CBS wa Marekani ambao matokeo yake yalichapishwa Jumapili iliyopita, umeonyesha kuwa, takriban robo tatu ya wapiga kura waliojiandikisha nchini Marekani wanaamini kuwa Rais Joe Biden hana afya ya kiakili inayomfanya astahiki kuchaguliwa tena kuongoza nchi katika kipindi cha miaka minne ijayo.
342/